Our History
Home | About JAI
Home | About JAI
JAI ilianza rasmi mwaka 2008 katika Msikiti wa Taqwa Mwananyamala. Msikiti ambao unapakana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala, Kinondoni, Dar es salaam. Ni zao la waumini wa Masjid Taqwa wakiwa katika Darsa ya baada ya sala ya Alfajir walikuwa wakiwatembelea wagonjwa na kuwaombea dua.
Hamasaya kuliendea jambo hili kiofisi ilitokana na ukweli kwamba ibada hii ilisahaulika na waislam kama alivyokuwa akifanya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kupelekea wagojwa wengi kukosa usaidizi. Hivyo Waumini wa Masjid Taqwa kwa kuzinduka na kukumbuka mafundisho sahihi ya kuwatembelea wagonjwa waliona na pamoja na mambo mengine yaliyowasukuma wasiache ibada hiyo kwani ina malipo makubwa sana mbele ya Allah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na wakaazimia kukumbusha umma wa kiislam hasa Watanzania na ikibidi ulimwengu wote kwa jumla. Ni katika kumi la mwisho la Mwezi Mtukufu wa Ramadhani 1429 tukiwa katika ibada ya Itikaf suala hili likawa ni azimio la Waumini wa Masjid Taqwa.
Suala la kuona wagonjwa ni ibada iliyokokotezwa ndani ya Uislamu. Waislamu walikuwa wakienda mmoja mmoja au kikundi kabla ya utaratibu rasmi. Baada ya kuazimia siku hiyo utaratibu wa kuwaona wagonjwa ikawa ni rasmi kwa maana watu walianza kwenda kwa utaratibu maalum na kutatua changamoto za wagonjwa mbalimbali.
Tulianza kwa kuwafuata wagonjwa waliokuwa wapweke kwenye vitanda vyao ambapo tuligundua kuwa aidha hawakuwa na ndugu wa kuwahudumia ama ndugu hawana taarifa kwa sababu ya ajali au dharura tofauti ama kutelekezwa na jamaa zao kutoka na hali ngumu ya kimatibabu. Kwa wagonjwa wasiokuwa na ndugu basi sisi tukawa ni ndugu na jamaa zao na sababu ya kurudisha tabasamu lao lililopotea kwa kuzidiwa na maradhi na upweke wa ndugu. Ilikuwa inasikitisha sana kuona kitanda kimoja kimezungukwa na watu hata kumi lakini kitanda cha jirani hakina ndugu hata mmoja. Mahitaji ya kifungua kinywa yakawa makubwa hivyo Ndugu yetu Sheikh Yahya Tatee (Amir wa JAI kwa sasa) akachukua jukumu la kutengeneza chai na uji nyumbani kwake.
Uongozi wa Msikiti baada ya kuona umuhimu wa harakati hizi uliamua kutenga muda wa baada ya sala ya alfajiri kila siku kuchangisha sadaka kwa ajili ya wagonjwa. Muitikio ulikuwa mkubwa na pale ilipopatikana dharura, mchango ulichangishwa Msikitini mara moja. Zoezi hili liliendelea kwa miezi kadhaa na ndipo tulipoamua kumkabidhi majukumu haya Amir Yahya Masao kutuongoza katika jukumu hili. Naye kwa moyo mmoja alilipokea jambo hili na baadae akamtambulisha kwetu ndugu Abdallah Saad ambaye kwa sasa ndie Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya JAI.
Zoezi liliendelea kushika kasi na kupelekea kuunganisha nguvu na misikiti ya jirani iliyopo Mwananyamala kisha kuendelea kutanuka kwa kupeleka huduma hii Hospitali ya Amana (Ilala) na Hospitali ya Temeke (Temeke) na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Kisha baadae huduma ya JAI ikatoka nje ya Dar es salaam kwenda kuhamasisha Waumini wa Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Pwani (Kibaha). kisha Morogoro na maeneo mengi ya Tanzania bara na baadae Visiwani.
Maeneo yote tuliyokwenda kuhamasisha kuanzishwa kwa JAI tulitumia nembo ya misikiti husika katika maeneo hayo. Baada ya kupata nguvu katika mikoa hii minne yaani DSM,Tanga, Kilimanjaro, Kibaha Pwani na Morogoro tuliamua kutayarisha Katiba itakayosimamia Taasisi yetu ya JAI. Katiba hii ilitayarishwa Markaz Gongo la Mboto kwa ndugu Arif Surya. Na baada ya Shura tulikubaliana kutumia jina la Jaamiyatul Akhlaquul Islaam (JAI).
Hapo ndipo tulipoanza kuipeleka kazi ya JAI mikoa mingine ya Tanzania Bara na Visiwani.